Nairobi, Kampala, Gaborone, London 16th November 2020:
Jopo la watu mashuhuri wanaofuatilia uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020 wanaendelea kulaani vikali kuzidi kuzuiliwa raia pamoja na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Tanzania.
Jopo hili linazisihi mamlaka nchini Tanzania kuzingatia haki na uhuru wa raia kuwasi-lisha maoni na malalamiko yao kwa njia ya haki na kulingana na katiba pamoja na sharia mbali mbali za kimataifa.
Jopo hili limetambua kwa masikitiko kuhusu kuendelea kuzuiliwa kwa viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa kote nchini Tanzania.Taarifa za kukamatwa viongozi wengi wa upinzani Tanzania bara na Zanzibar ni ishara ya ukiukaji haki za kibinadamu na kuvunjwa mikataba ya kimataifa kuhusu haki nchini humo.
Jopo hili limesikitishwa na hatua ya kushitakiwa kwa wanachama kadhaa wa vyama vya upinzani kwa tuhuma za uhalifu wa kiuchumi. Ripoti za hivi karibuni kuhusu kupigwa risasi hadharani kiongozi wa ACT Wazalendo huko Zanzibar zinatishia kulitumbukiza taifa katika machafuko ya baada ya uchaguzi kinyume na matakwa ya demokrasia. Mazingira kama hayo ni kinyume na sheria pamoja na.mikataba ya kimataifa kwa mfano Kipengele cha 13 cha Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora pamoja na Kipengele cha 25 cha Mkataba wa ICCPR.
Kipengele cha 32 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai za Tanzania kimeelezea kuhusu haja ya maafisa wa polisi kuwaachilia huru kwa bondi washukiwa watakaokosa kufikishwa mahakamani saa 24 baada ya kukamatwa.
Jopo hili limesikitishwa na ukiukwaji wa sheria hii na ripoti za washukiwa kuendelea kizuiliwa. Jopo hili linazitaka mamlaka nchini Tanzania kukomesha ukiukaji huu wa sheria kwa kuwaachilia au kuwashtaki washukiwa wa makosa ya kisiasa.Jopo hili pia limesikitishwa na ripoti za baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wa masuala ya kiraia kutoroka Tanzania kwa madai ya kuhofia usalama wao.
Ripoti hizo ni ishara ya wanasiasa au wanaharakati kulengwa kutokana na misimamo yao kisiasa. Ripoti hizi zinatishia kuhujumi haki za raia kufurahia amani uhuru na umoja wa kitaifa.Katika mazingira ya kidemokrasia raia na wanasiasa sharti waruhusiwe kujieleza na kuchagua viongozi wao bila uoga au upendeleo.Tanzania sharti ilinde haki za raia wote wakiwemo wapinzani kutekeleza uhuru na haki zao kwa mujibu wa kipengele 12 cha katiba.
Kuendelea kufurahia haki za kimsingi zikiwemo kuweza kujieleza, kutangama na kujihusisha ni kiini cha masuala makuu yanayoambatana na kipengele cha 3 cha katiba ya Tanzania. Ili kuweza kutimiza malengo ya kidemokrasia ni sharti mamlaka nchini humo kutenda kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia katiba na mikataba ya kitaifa iliyoidhinisha.
Tunaisihi jumuiya kimataifa kuungana nasi katika kuishinikiza Tanzania kulinda haki na uhuru wa wananchi kulingana na sheria.Tunaiomba jamii ya kimataifa pia kumsihi raia John Pombe Magufuli kuhakikisha amani na utulivu nchini Tanzania kwa kuzingaria sheria na haki.